Waziri awatoa hofu wakulima wa korosho wanaosubiri malipo

|
Waziri wa Kilimo, Josephat Hasunga akitolea ufafanuzi kinachofanyika kwa sasa

Wakulima wa zao la korosho 34,938 wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 35.5 kufuatia uhakiki wa mauzo yao ya korosho katika vyama vya msingi 157 kati 504.

Waziri wa Kilimo, Josephat Hasunga amesema hayo alipozungumza na watendaji mbalimbali wanaosimamia zao la korosho kutoka mikoa ambayo zoezi la ukusanyaji na uuzaji korosho linafanyika.

Waziri Hasunga amesema, kumekuwepo na maneno mengi kuhusu kinachooendelea katika zoezi la ulipaji, ambapo ametolea ufafanuzi kuwa hadi sasa Mtwara yenye vyama 212 tayari vimeshakikiwa na kwamba wakulima wake wanataraji kuingiziwa malipo yao hivi karibuni sanjari na mikoa mingine ya Lindi, Ruvuma na Pwani.

Pamoja na idadi kubwa ya malipo kufanyika, viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika wameiomba Serikali kuwalipa wadhamini wa magunia na wasafirishaji wa korosho ili zoezi la usombaji wa korosho ghafi liweze kuendelea bila ya kusimama.

Akizungumzia suala hilo, Mohamed Nassoro, Meneja mkuu Tanecu amesema, iwapo suala hilo halitachukuliwa kwa uzito linaweza kuzua mgogoro na kukimbiza wafanyabiashara wa magunia na hivyo kuathiria mauzo ya zao hilo kwa msimu ujao.

Naye Mwenyekiti wa CORECU, Rajabu Ngonomi amemuomba waziri Hasunga kuharakishwa kwa zoezi la usombaji wa korosho mkoani Pwani, ili kuzinusuru na tishio la mvua zinazotarajiwa kunyesha na kuziomba mamlaka husika kuwa na kauli moja.

Serikali imeendelea na malipo ya wakulima wa zao la korosho katika mikoa mitatu ya kusini ambapo kwa upande wa Mkoa wa Pwani zoezi la uhakiki lilianza jana.

Biashara
Maoni