Waziri aweka wazi mpango wa kumtumia Samatta katika utalii

|
Mbwana Samatta na Flavian Matata ambao Waziri wa Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla ambaye amewatangaza kuwa mabalozi wa Utalii wa nje ya nchi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, ameweka wazi kuwa ili kukuza utalii tayari wameshaanza mazungumzo na Klabu ya KRC Genk anakochezea Mtanzania Mbwana Ally Samatta (Samagoal10) ili kuweza kutangaza utalii nchini Ubelgiji.

Waziri Kigwangalla amesema hayo mapema wiki hii alipotumia mtandao wake wa Kijamii wa Twitter kujadiliana na wadau mbalimbali wa utalii namna Serikali kupitia wizara yake ilivyojipanga kutangaza vivutio vya utalii nchini kupitia mbinu mbalimbali.

Waziri Kigwangalla amesema kwa kuanza wameshawabaini mabalozi kadhaa watakaoweza kusaidia juhudi hizo wakati mkakati mahsusi kwa ajili ya kujitangaza kwenye nchi mbalimbali ukiendelea.

Mbali na kuweka mipango juu ya Samatta, Waziri huyo pia amemshukuru mwanamitindo wa Kimataifa, Flaviana Matata kukubali uteuzi wake wa kuwa Balozi wa hiari wa Utalii nchini.

"Tunakushukuru na kukupongeza Flaviana Matata kwa uzalendo wako. Tutakupa hati ya shukrani na pia tunakupa Safari ya siku Tano (5) kwenye maeneo ya vivutio siku yoyote utakayokuwa tayari." Aliandika Waziri Kigwangalla.

Pamoja na hayo Waziri Kigwangalla amesema kwamba tayari amekwisha kamilisha kazi ya kubuni kauli mbiu ya #TanzaniaUnforgettable ambayo itaitambulisha nchi kwenye masoko ya utalii.

Amesema, awali Tanzania ilikuwa inapokea watalii  milioni 1.2 wakati akiingia madarakani, lakini sasa amesema, wamejipanga upya na sasa wanauhakika baada ya miaka mitatu wamejiwekea malengo ya kufikia watalii milioni mbili huku akijipongeza kwa mwaka jana kuwa watalii wa ndani na Kenya walikuwa wengi zaidi.

Hata hivyo kupitia ukurasa wake huo, waziri Kigwangalla alipokea ushauri na mawazo mbalimbali kutoka kwa wadau wa ndani na nje wa utalii huku wengine wakimpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya sambamba na kushauri uwepo mijadala ya kuboresha zaidi sekta hiyo na kutatua changamoto za utalii zilizopo.

Utalii
Maoni