Waziri Hasunga azipa 'mtihani' NFRA na Bodi ya mazao mchanganyiko

|
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akiangalia maendeleo ya ujenzi wa maghala na vihenga vya kisasa mkoani Ruvuma huko Songea

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko zimetakiwa kuandaa mikakati ya haraka kwa kuanisha jinsi watakavyo nunua mazao ya wakulima nchini.

Wakati NFRA imetakiwa kuainisha namna ya kununua nafaka za wakulima kwa upande wa Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko yenyewe imetakiwa kujikita katika ununuzi wa mazao mbalimbali ya wakulima ikiwa ni pamoja na kutafuta masoko ya mazao ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa jana Januari 5 na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa.

Alisema kuwa wizara yake imekuwa ikihamasisha wakulima nchini kuzalisha kwa wingi mazao kwa ajili ya chakula na biashara lakini inapofika hatua ya kuuza bei zinakuwa ndogo jambo ambalo serikali haitalifumbia macho kamwe.

Pamoja na mambo mengine, waziri Hasunga ameupongeza Uongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa (Silos) katika maeneo nane ya kanda saba za wakala ambapo ujenzi huo utaongeza uwezo wa kuhifadhi mahindi kutoka tani 251,000 za sasa hadi tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

Mradi huo wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi umeanza kujengwa katika Manispaa ya Songea (Ruvuma), Dodoma, Mpanda (Katavi), Makambako (Njombe), Mbozi (Songwe), Sumbawanga (Rukwa), Shinyanga Mjini (Shinyanga), na Babati (Manyara) ambapo Serikali ya Tanzania na ya Poland zilisaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na shilingi bilioni 124, kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.

Hasunga amesema kuwa punde utakapokamilika ujenzi wa maghala na vihenge hivyo utapunguza gharama mbalimbali zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya kununua madawa ya kufukiza mahindi sambamba na gharama za kununua magunia ya kuhifadhia mahindi.

Katika hatua nyingine Waziri huyo amemtaka Kaimu Mtendaji Mkuu wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Vumilia  Zikankuba kuweka msisitizo zaidi wa kununua nafaka ya mahindi kwani katika kipindi chake serikali haitatoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mahindi badala yake NFRA ijipange kibiashara ili iweze kununua nafaka nyingi na kujiendesha.

Vilevile, ameutaka Wakala wa majengo Tanzania (TBA) kusimamia kwa weledi mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwanufaisha wananchi.

Kilimo
Maoni