Waziri mkuu New Zealand atangaza Ijumaa kuwa ya maombolezo

|
Waumini na wananchi wa New Zealand wakionesha majonzi yao kwa waliouawa kwenye shambulio la kigaidi la kupigwa risasi

Waziri mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern ametangaza kwamba ifikapo Ijumaa kutakuwa na ukimya wa dakika mbili (2) nchi nzima kama ishara ya kuwakumbuka watu 50 waliouawa katika shambulio la kigaidi ndani ya misikiti miwili mjini Christchurch.

Hatua hiyo itaashiria wiki moja tangu kutokea kwa shambulio hilo lililotekelezwa na kijana mwenye umri wa miaka 28 ambaye tayari amefikishwa mahakamani na huenda mashtaka yake yakaongezwa zaidi. 

Tayari mazishi ya watu waliuoawa katika tukio hilo la kigaidi yameanza kufanyika jana yakiwa yamechelewa kutokana na uchunguzi wa vinasaba na ndugu kuwatambua wapendwa wao ambapo mpaka sasa miili 12 imeshatambuliwa.

Waziri Mkuu wa New Zealand amesema mbali na ukimya wa Ijumaa, siku hiyo pia itakuwa ni ya maombi maalumu yatakayotangazwa mbashara na vyombo vya habari vya kitaifa.

"Nafahamu kwamba kila mmoja ana shauku ya kuonyesha upendo na kuwatia moyo Jamii ya kiislam, wanaojiandaa kurejea misikitini hasa kwa siku ya Ijumaa wa swala ya kitaifa. Kuna utayari pia kwa watu wa New Zealand kufanya kumbukumbu ya wiki moja tangu kutokea kwa shambulio hilo baya la kigaidi. Kwa kutambua hayo, kutakuwa na ukimya wa dakika mbili (2) siku ya Ijumaa. Na tutatangaza mbashara kupitia Radio na TV ya Taifa."

Maisha
Maoni