Test
Marekani waungana kuushtaki utawala wa Trump

Majibo 16 nchini Marekani yakiongozwa na California yameungana kuushtaki utawala wa Rais Donald Trump kwa uamuzi wake wa kutangaza hali ya dharura kwa lengo la kukusanya fedha za ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Kesi hiyo imewasilishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kaskazini katika Jimbo la California, siku kadhaa baada ya Trump kutangaza hali ya dharura inayompa mamlaka juu ya bunge na kujipatia fedha kwa ajili ya ujenzi huo ambayo ni ahadi kubwa aliyotoa wakati wa kampeni yake.

Hata hivyo Wana Democrat wameapa kupinga hatua hiyo kwa udi na uvumba.

Nje ya Ikulu ya Marekani (White House) mamia ya watu wamekusanyika wakishikilia herufi zilizounda maneno 'Stop Power Crab' kwa maana ya shinikizo kwa Rais Trump kuacha matumizi mabaya ya Madaraka yake.

Kesi hiyo iliyowasilishwa mahakamani inalenga pia kuweka zuio kwa Rais Trump kuendelea na tangazo lake la hali ya dharura ya Kitaifa mpaka pale kesi ya msingi itakapokamilika.

Wakati huo huo Rais Donald Trump ameendeleza kampeni zake za kutafuta kuungwa mkono kwa kiongozi wa Upinza wa Venezuela Juan Guaido aliyejitanza kuwa Rais wa mpito nchini humo.

Akiwa katika katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Florida, Jimbo la Florida ambako wanaishi wavenezuela wengi nchini Marekani, Rais Trump amesisitiza kumtambua Juan Guaido na kuzipuuza sera za Kisoshalisti za Rais Nicolas Maduro.

Hata hivyo Chama cha Kisoshalisti cha Venezuela kimeitisha maandamano ya kuiunga mkono Serikali ya Maduro, huku kiongozi wake Chief Diosdado Cabello akiigiza namna wabunge wa Bunge la Ulaya walivyofukuzwa nchini Venezuela mara tu baada ya kuwasili nchini humo kwa mwaliko wa Kiongozi wa upinzani Juan Guaido.

Hali ya amani yaanza kurejea Haiti

Shuguli za kijamii na za Serikali zimeanza kurejea taratibu katika Kisiwa cha Haiti baada ya wiki moja ya maandamano ya mamia ya watu yaliyoambatana na vurugu za kumshinikiza Rais Jovenel Moise kujiuzulu.

Raia katika Mji mkuu wa Port-au-Prince wameonekana mitaani wakitafuta chakula, maji na mafuta huku maafisa wa polisi na watumishi wengine wa Umma wakisafisha mitaa iliyoathiriwa na maandamano hayo.

Raia wa Haiti wana malalamiko ya kupanda mara dufu kwa bei za bidhaa na wakidai ufisadi umekithiri ndani ya Serikali yao.

Hata hivyo Rais Moise amekataa kuachia madaraka, licha ya Waziri wake Mkuu, Jean-Henry  mwishoni mwa wiki kusema kwamba amekubali kupunguza bajeti za Serikali kwa asilimia 30.

Maeneo yatakayoathiriwa na punguzo hilo la bajeti ni safari za maafisa wa Serikali na marupurupu mengine kama ya gharama za simu.

Dunia yaadhimisha Siku ya Wapendanao

Wakati Dunia leo ikisheherekea siku ya wapendanao maarufu kama Valentine's Day, nchi mbalimbali zimesheherekea siku hii katika tamaduni zao na aina tofauti kulingana na jamii husika.

Licha ya Siku hii kuwa na historia ya kiimani lakini kwa sasa imegeuka kuwa siku ya familia, wapendanao na hata ya kibiashara.

Katika sehemu kadhaa duniani siku hii ya Valentine ambayo huadhimishwa kila Februari 14 imeshuhudiwa watu wakitumiana maua, marafiki na familia wakijumuika kwa chakula cha pamoja na hata kubadilishana zawadi.

Lakini kwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, katika mitandao ya kijamii watu na marafiki mbalimbali wametakiana heri katika kusheherekea siku hii kwa kutumiana jumbe mbalimbali za upendo na wengine kutumiana zawadi zilizopambwa kwa rangi nyekundu.

Je kwa upande wako wewe leo umeiathimishaje siku hii?

Airbus kusitisha uundaji ndege kubwa za A380 ifikapo 2021

Kampuni kubwa ya kuunda ndege barani Ulaya, Airbus, imesema itasitisha kuunda ndege kubwa zaidi ya abiria duniani A380.

Katika taarifa yake, Airbus imesema ifikapo mwaka 2021 itakamilisha uundwaji wa ndege za mwisho na kuzikabidhi kwa wateja.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Shirika la Ndege la Emirates, kutangaza kuwa litapunguza idadi ya ndege za A380 inazohitaji kununua kutoka 162 mpaka 123.

Ikumbukwe kuwa Emirates ndiyo mteja mkubwa zaidi wa A380 duniani.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 550 iliyogharimu mabilioni ya dola kuibuni na kuiunda, imeshindwa kupata wateja wengi katika soko ambalo hivi sasa linaegemea zaidi katika ndege zenye ukubwa wa kati.

Iran waadhimisha kumbukumbu ya miaka 40 ya mapinduzi

Raia wa Iran wameandamana nchi nzima kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.

Sikukuu hii inakuja kukiwa na mvutano kati ya Iran na Umoja wa Mataifa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa Marekani kutoka katika mkataba wa nyuklia wa Tehran mwezi Mei mwaka jana na kuiwekea vikwazo vipya Iran mwezi Novemba.

Mamia ya waandamanaji wameonekana leo, Jumatatu katika mitaa ya mjini Tehran na kisha kuhutubiwa na Rais wao, Hassan Rouhani ambaye amesema mapinduzi hayo ni ya kuenziwa muda wote kwa kuwa yameifanya Iran kuondoka mikononi mwa wakoloni.

Pamoja na hayo amesisitiza kuwa wataendelea na mipango yao ya kujihami kwa silaha za kivita dhidi ya maadui zao kwa kuwa hawahitaji kuomba ridhaa ya mtu yeyote kufanya hivyo.

Waandamanaji waendelea kupinga rushwa mitaani Haiti

Maelfu ya waandamanaji wameendelea kusalia katika mitaa ya mji mkuu wa Haiti wa Port-au-Prince huku wakikabiliana na Polisi wakipinga rushwa na hali ngumu ya kiuchumi nchini humo.

Waandamanaji wamefunga baadhi ya barabara kwa kuchoma matairi na kuteketeza magari kwa madai ya kuchoshwa na utawala mbovu wa kisiwa hicho kilichoko ukanda wa Caribbean na Pasific.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mtu mmoja alikufa katika majibizano ya waandamanaji na polisi baada ya waandamanaji kushambulia kwa mawe nyumba ya Rais wa Haiti, Jovenel Moise.

Waandamanaji hao wamekuwa na hasira juu ya Mfumuko wa Bei wa Kiwango cha kupindukia unaozidi kuongezeka na kushindwa kwa Serikali kuchukua hatua dhidi ya ufisadi katika miradi ya mafuta nchini Haiti.

Maduro atangaza utayari wa kijeshi dhidi ya Marekani

Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro amejitokeza katika Televisheni ya Taifa na kutangaza utayari wa jeshi lake kukabiliana na aina yoyote ya uvamizi ama mashambulizi ya Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Kauli ya Maduro imekuja baada ya kutembelea viunga vya mazoezi ya kijeshi akiambatana na waziri wa Ulinzi na makamu wa Rais katika Jimbo la Miranda nchini Venezuela.

Mazoezi hayo ya kivita yamehusisha majaribio ya mifumo ya kudhibiti mashambulizi kutoka angani na silaha nyingine za kivita, lakini Maduro amesema bado majaribio muhimu hayajafanyika. 

“Vitisho vya Marekani vimetulazimisha kujiandaa kwa uhakika ili kulinda haki na amani ya nchi, kulinda utu wa watu wa Venezuela, uhuru kamili kama Taifa, kulinda uhuru wa kuishi katik karne hii ya 21 kama Taifa huru lenye watu huru.” Alisema Maduro.

Kiongozi huyo wa kisoshalisti anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Kiongozi wa Upinzani,  Juan Guaido kijana mwenye umri wa miaka 35 na Raisi wa Kambi ya upinzani Bungeni aliyejitangaza kuwa Rais wa mpito nchini Venezuela mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu.

Licha ya shinikizo la kuondoka madarakani kwa madai ya kushinda isivyo halali katika uchaguzi uliomweka madarakani, lakini Maduro ameshikilia msimamo wake wazi kwamba hataondoka madarakani kirahisi.

Guaido ameomba msaada wa kibinadamu kama dawa na chakula kutoka mataifa yanayomuunga mkono, lakini Maduro amekataa misaada hiyo kuingia nchini humo kwa madai kuwa Venezuela sio ombaomba.