Yanga, Azam zabanwa Ligi Kuu Tanzania Bara

|
Lilipopatikana bao la kusawazisha la Alliance FC.

Azam FC, imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Alliance katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ilibidi Azam FC iweze kusubiri hadi dakika ya 79 kuweza kupata bao la uongozi, lililofungwa na Joseph Mahundi, aliyeingia dakika ya 76, kuchukua nafasi ya Ramadhan Singano na alifunga bao hilo kiustadi akiunganisha krosi ya Chirwa.

Dakika ya 90 Alliance ilisawazisha kupitia kwa Dickson Ambundo, akimalizia mpira uliogonga mwamba kufuatia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Israel Patrick.

Azam walionekana kulalamikia bao hilo wakidai kuwa beki wao, Agrey Moris alisukumwa kabla ya kufungwa lakini, mwamuzi Abubakar Mturo (Mtwara) na Msaidizi namba moja, Mohamed Mkono (Tanga), waliamuru kuwa bao halali.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika, kipa wa Azam FC, Razak Abalora, alioneshwa kadi nyekundu kufuatia kadi ya pili ya njano iliyosababishwa na lugha ya kutoridhishwa na maamuzi aliyoitoa kwa mwamuzi huyo.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 48 katika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na mchezo mmoja mkononi, ikizidiwa pointi saba na kinara Yanga aliyefikisha 55 kufuatia suluhu yake ya jana dhidi ya Singida United.

Matokeo ya mechi nyingine zilizopigwa Jumatano hii ni kama ifuatavyo.

Singida United 0-0 Yanga.

Lipuli 1-0 KMC (Miraji Athuman 11’).

Kagera Sugar 0-1 Mbeya City (Victor Hangaya 15’).

Stand United 2-0 Ndanda SC (Six Mwasekaga 9’, 23’).

TZ Prisons 2-1 Mbao FC (Salum Kimenya 12’, Adam Adam 20’ : Amos Charles 34’).

JKT Tanzania 3-1 Biashara United (Ally Shiboli 2’, Samwel Kamuntu 20’, Ally Bilaly 85’ : Wazir Jr. 65’)

Ligi hiyo inaendelea leo kwa michezo miwili ambapo Coastal Union watakuwa nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting huku Simba wakiwakaribisha mwadui FC kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

TPL
Maoni