Latest News
KMC yazidi kujisuka, yanasa kiungo kutoka Kenya

Timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) imeendelea kujipanga kwaajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kumsajili kiungo mshambuliaji, Abdul Hillary Hassan kutoka Tusker FC ya Kenya.

Afisa Habari wa KMC, Walter Harrison amesema mchezaji huyo ambaye ni Mtanzania, amejiunga rasmi na klabu ya KMC FC kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Kiungo huyo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 23, urefu wa futi 6 na uwezo wa kutumia miguu yote kwa ufasaha, anakuwa mchezaji mpya wa tano kusajiliwa KMC baada ya kipa Juma Kaseja na mabeki Aaron Lulambo, Sadallah Lipangile na Ali Ali. 

Latest News
Kombe la Kagame kufanyiwa mageuzi makubwa

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepanga kuongeza timu shiriki katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) msimu ujao na kufikia timu 16.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye amesema timu hizo 16 zitakuwa katika makundi manne.

Sanjari na hilo Musonye amesema CECAFA inatarajia kubadili kalenda yake ya mashindano ili kufuata ratiba ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) na kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Aidha Musonye amesema kuna uwezekano mkubwa wa nchi za Malawi, Zambia na Congo DR kujiunga na CECAFA baada ya mataifa hayo kuomba kuandaa fainali za Kombe la Kagame msimu ujao wa 2018/2019.

Latest News
Netiboli Tanzania yatolewa kifungoni

Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kimefunguliwa na Chama cha Netiboli cha Kimataifa (FINA) na sasa kitakuwa huru kushiriki michuano ya kimataifa kwa klabu na timu za taifa.

Kufunguliwa huko kwa CHANETA kumekuja baada ya kukubaliwa ombi lao na FINA huku wakitakiwa kulipa ada ya malimbikizo ya uanachama ya miaka mitatu ambayo kila mwaka hugharimu kiasi cha dola 1,500 za Marekani.

Mwenyekiti wa CHANETA, Dkt. Devota Marwa amesema watalipa ada hiyo wakati wa mashindano ya kufuzu kwa michuano ya Afrika itakayofanyika nchini Zambia mwezi ujao ila Tanzania haitapeleka timu msimu huu.

Latest News
Feisal Salum atua rasmi Singida United

Klabu ya Singida United imefanikiwa kuinasa saini ya mchezaji, Feisal Salum Abdallah ‘FEI TOTO’ kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea JKU ya Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa leo, Alhamisi na Singida United imeeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo umekubaliana na uongozi wa JKU kuhusu ada ya uhamisho ambapo Singida United wamekubali kulipa gharama za kufidia miaka miwili ya mkataba ambao mchezaji huyo alikuwa ameubakiza katika klabu ya JKU.

Huu ni mwendelezo wa kukisuka kikosi cha timu hiyo chini ya kocha Hemedi Selemani Morocco wakiwa tayari wamewasajili Habib Kiyombo kutoka Mbao FC, Tibar George kutoka Ndanda FC, Eliuter Mpepo kutoka Tanzania Prisons na David Kisu kutoka Njombe Mji.

Putin aitaka Kamati ya Olimpiki 'kulisafisha' Urusi Kimataifa

Rais wa Urusi, Vladimir Putin amewataka viongozi wa michezo nchini humo kurejesha hadhi ya nchi hiyo Kimataifa huku akiwaomba kuanzisha utamaduni wa kutomvumilia mtu yeyote anayejihusisha na matumizi ya dawa haramu michezoni.

Rais Putin ameyasema hayo muda mfupi kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji kura kumchagua kiongozi wa juu wa Kamati ya Olimpiki nchini Urusi.

Taarifa iliyotolewa na Rais huyo imesema kuwa ni muhimu kulisafisha taifa lao na kurejesha hadhi na jitihada za wanariadha wake kimataifa huku akiwataka kutoa kipaumbele kwa mabadiliko ya mfumo wa kiutendaji unaolenga kupinga matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Licha ya kuwa hawajawahi kukiri popote tuhuma za taifa hilo kukingia kifua matumizi ya dawa hizo kwa wanariadha walioshiriki mashindano mbalimbali kati ya mwaka 2011 na 2015, bado Rais huyo ameonekana kuchukizwa na taifa lake kunyooshewa vidole.

Wanamichezo 60 kutoka Ulaya washiriki mbio za hisani Kilimanjaro

Jumla ya wanamichezo 60 kutoka nchini Ujerumani na Uswizi wameshiriki mbio za hisani zinazolenga kuchangia fedha kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu hapa nchini.

Wanamichezo hao wameungana na wenzao wa Tanzania kushiriki mchezo wa kukimbia, kutembea na mbio za baskeli ambayo imefanyika katika kijiji cha Masama Roo wilayani Hai.

Mkurugenzi wa shirika linalo hudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu Agnes Stanley amesema michezo hiyo ya hisani inafanyika kwa mara ya kwanza nchini ili kuwaleta pamoja walezi na wafadhili wa watoto wapatao 91,000 wanaolelewa na shirika hilo.

Ngome yaondoka na makombe mawili CDF Cup

Timu za mpira wa kikapu na wavu za Ngome zimetwaa ubingwa wa michezo ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup), baada ya kuzifunga timu za JKT katika michezo iliyochezwa leo kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mpira wa kikapu, Ngome iliifunga JKT kwa pointi 78 kwa 62  wakati katika mpira wa wavu Ngome pia ilishinda kwa seti 3-2 dhidi ya JKT.

Timu ya Nyika imeshika nafasi ya tatu katika mpira wa miguu baada ya kuifunga Navy kwa penati 5 kwa 4 baada ya kutoka suluhu katika muda wa kawaida.

Fainali ya soka ya Kombe la Mkuu wa Majeshi inatarajiwa kuchezwa Ijumaa hii saa 4:00 asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kwa kuzikutanisha timu za JKT na Ngome.

Michezo hiyo ya Kombe la Mkuu wa Majeshi inafikia tamati kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa Uhuru na itaonyeshwa moja kwa moja na Azam Sports 2.

Mwanariadha John Stephen Akhwari amfunda JPM

Mwanariadha wa zamani wa Tanzania John Stephen Akhwari amemshauri Rais Magufuli kuwekeza kwenye sekta ya michezo kwa kujenga shule na vituo vya kukuzia vipaji.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Azam TV, Akhwari amesema kama serikali haina uwezo itafute wafadhili ili angalau vituo hivyo vijengwe kwenye kila kanda kwaajili ya kuzalisha wachezaji bora katika michezo mbalimbali ikiwemo soka, riadha, ngumi n.k.

Akhwari ambaye anakumbukwa zaidi kwa kupambana hadi kumaliza marathon mwaka 1968 nchini Mexico, amesema kwa siku za karibuni Tanzania imekuwa haifanyi vizuri kwenye riadha ikiwa ni pamoja na wanariadha kushindwa kumaliza mbio kutokana na kukosa uzalendo na kujali zaidi maslahi.

“Vijana wa sasa wengi wao hawana uvumilivu, halafu wanaangalia fedha, akiona ameshindwa, anaona kwanini aendelee na fedha hana, uzalendo kama ule, haupo.” amesema mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 80.

Mzee Akhwari amezungumza hayo akiwa amerejea nchini kutoka nchini Marekani alikokwenda kuchukua tuzo ya heshima aliyotunukiwa na Watanzania waishio katika jimbo la Dallas kwa kutambua mchango wake kwa taifa.

Wengine waliopata tuzo hiyo iliyopewa jina la 'TUNU ADIMU' ni Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Nelson Mandela.