Test
Mwanariadha wa Ethiopia aliyemakinisha dunia wakati wa Olimpiki azawadiwa na serikali yake

Mwanariadha wa Ethiopia aliyeifanya dunia kumakinika na hali ya migomo na maandamano nchini humo wakati akimaliza mbio za Olimpiki zilizofanyika nchini Brazili kwenye jiji la Rio de Janeiro hatimaye amezawadiwa na serikali ya nchi yake.

Feyisa Lilesa, ambaye amepewa $17,000 (TZS 35m), amesema jitihada zake na magumu aliyopitia hatimaye yamefanikiwa kutokana na kuwepo kwa aina za uhuru zilizokuwa zikipiganiwa na watu wa kabila la Omoro.

Mwanariadha huyo alimaliza mbio hizo akiwa kwenye nafasi ya pili na wakati wa kumaliza mbio hizo za mwaka 2016 alipishanisha mikono yake juu ya usawa wa kichwa chake kuashiria kufungwa minyororo ikiwa ni alama ya kukandamizwa kwa waandamanaji nchini mwake.

Aliendelea kusalia uhamishoni kwa miaka miwili zaidi akisema maisha yake yalikuwa hatarini.

Usain Bolt aachana na soka, ahamia kwenye biashara

Mfalme wa mbio fupi duniani, Usain Bolt amethibitisha rasmi kuachana na michezo yote ikiwemo soka na sasa ameamua kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa ulimwenguni.

Mshindi huyo mara nane wa medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki, amesema maisha ya kiuanamichezo yamefikia tamati kwa upande wake hivyo ameamua kujikita katika miradi mingine.

Bolt mwenye umri wa miaka 32 amekuwa akijifua katika Klabu ya Central Coast Mariners kwa kipindi cha miezi miwili mwaka 2018.

Hata hivyo, Mjamaica huyo alilazimika kuachana na Mariners mwezi Oktoba baada ya uongozi wa klabu kushindwa kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kuingia naye mkataba wa ajira kama mchezaji rasmi wa kandanda.

Baada ya kustaafu riadha mwaka 2017, Usain Bolt alihakikisha anatimiza ndoto yake ya kuwa mchezaji soka na amefanikiwa kuacha kumbukumbu ya kuwahi kuzifumania nyavu mara mbili katika mechi mbili za kirafiki alizoichezea Mariners.

Tanzanite Marathoni: Wanariadha 3,000 kuchuana

Kwa mara ya kwanza maelfu ya wafukuza upepo kutoka ndani na nje ya nchi ya Tanzania watakimbia mbio kwa kuzunguka ukuta wa machimbo ya madini ya Tanzanite yaliyoko Mirerani katika mbio zilizopewa jina la Tanzanite International Marathoni.

Mashindano hayo yatakayohusisha mbio za kilometa 21 (Half Marathoni) na za kilometa 5 (Fun Run) zitafanyika Januari 27 mwaka 2019 na zinalenga kutangaza madini ya Tanzanite pamoja na kuibua vipaji vya wanariadha.

Waandaji wa mbio hizo chini ya Mwenyekiti wao, Charles Mnyalu wamesema licha ya mbio hizo kutoa ajira pia ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kwa hatua alizochukua kudhibiti rasilimali za madini kwa kujenga ukuta huo wa Mirerani.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zephania Chaula, akizungumza wakati wa utambulisho wa mbio hizo amesema serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha mbio hizo huku akiwataka wadau wa michezo kuanzisha mashindano mbalimbali ili kutoa fursa ya ajira kwa wakazi wa mji mdogo wa Mirerani na maeneo mengine nchini.

Takribani wanariadha 3,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki mashindano hayo huku milango ya usajili ikiwa imefunguliwa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro pamoja na Manyara. 

Arusha yafunika Dodoma Marathon 2018

Mbio za Dodoma Marathon zimefanyika leo jijini Dodoma zikishirikisha wakimbiaji mchanganyiko wakiwemo wanariadha wakubwa kutoka ndani nan je ya mkoa huo.

Mbio hizo zilikuwa katika makundi mawili, yaani Kilomita 21 na Kilomita 42 wanawake kwa wanaume ambapo washiriki kutoka mkoa wa Arusha ndiyo waliofanikiwa kuibuka washindi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mbio hizo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka wanariadha wa Tanzania kutobweteka na mazoezi, badala yake wapambane na kushiriki mbio mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Katika mbio hizo, upande wa wanaume Marathon, John Karori kutoka Arusha alishika nafasi ya kwanza akitumia muda wa saa 2 dakika 28 na sekunde 42, mshindi wa pili ni Tumaini Leku naye kutoka Arusha akitumia muda wa saa 2 dakika 31 na sekunde 22.

Wengine walioshinda kwa wanaume ni Marco Silvester na wa pili Fabian Joseph huku Gelvas Mayo akishika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa wanawake, Kilomita 42 mshindi ni Angelina Joseph kutoka Arusha na wa pili ni Neema Kisuda huku wa tatu akiwa ni Flora Yuda pia kutoka Arusha.

Wanariadha wa Tanzania wang'ara Canada na Japan

Mwanariadha wa Tanzania, Augustino Sulle kutoka mkoani Manyara, amevunja rekodi ya taifa ya marathon iliyokuwa ikishikiliwa na mkongwe Juma Ikangaa tangu mwaka 1989.

Sulle ametumia saa 2 dakika 07 na sekunde 45.9 kwenye mashindano ya Toronto Waterfront Marathon huko Canada na kushika nafasi ya pili nyuma Cam Levins wa Canada ambaye naye amevunja rekodi ya nchi yake.

Katika mbio hizo, bingwa wa Olimpiki ya 2012, Stephen Kiprotich wa Uganda ameshika nafasi ya 7.

Rekodi ya Juma Ikangaa ilikuwa saa 2, dakika 8 na sekunde 1 kwenye New York Marathon, muda ambao ulikuwa bora duniani mwaka huo.

Katika mashindano mengine yaliyofanyika huko Nagai Japan, wakimbiaji 7 kati ya 8 wa Tanzania, wamefanya vizuri na kutoa matumani kwa taifa kuelekea Olimpiki 2020.

Mkenya aweka rekodi mpya mbio za Berlin Marathon

Mwanariadha wa Kenya Eliud Kipchoge ameweka rekodi mpya ya dunia ya mbio za Marathon za Berlin kwa kumaliza mbio katika muda wa saa 2, dakika 1 na sekunde 39.

Kipchoge amevunja rekodi ya Berlin Marathon iliyodumu kwa miaka minne iliyowekwa na Mkenya mwenzie Dennis Kimetto aliyekimbia kwa saa 2, dakika 2 na sekunde 57.

Nafasi ya pili katika mbio hizo imeshikwa na Amos Kipruto na Wilson Kipsang wote ni raia wa Kenya.

Rekodi nne za dunia za mwisho katika mbio za Berlin zimewekwa na kuvunjwa na Wakenya 2011 Patrick Makau aliweka rekodi ya kukimbia kwa (2:03:38) 2013, Wilson Kipsang akavunja rekodi ya Makau na kuandikisha rekodi yake ya kukimbia kwa (2:03:23).

Rekodi ya Kipsang ilidumu kwa mwaka mmoja pekee kwani mwaka 2014 Dennis Kimetto alivunja rekodi hiyo kwa kukimbia saa  (2:02:57)

Rekodi ya Kimeto imedumu kwa miaka minne kabla ya Kipchoge kuivunja Rekodi hiyo Jumapili hii.

Kwa kuvunja rekodi hiyo Kipchoge anatambulika kama mwanaridha bora wa mbio ndefu kwa muda wote duniani.

Kipchoge amekua mtawala wa Berlin Marathon ikiwa ni mara ya tatu kuibuka mshindi kwenye mbio hizo zinazofanyika kila mwaka nchini Ujerumani.

Mwaka 2015 Kipchoge aliibuka mshindi kwa kukimbia kwa saa 2 dakika 40 na sekunde 01, mwaka 2017 Kipchoge akaibuka na ushindi wa saa 2 :03:34 na mwaka huu ameivuka tena ushindi na kwa kuvunja rekodi ya dunia.

Mkenya mwingine, Gladys Cherono ameshinda upande wa wanawake  kwa kukimbia kwa saa 2, dakika 18 na sekunde 10, akiwatangulia Waethiopia Ruti Aga na Tirunesh Dibaba ambaye alikuwa akipewa kubwa ya kushinda.

BMT yapewa nguvu kisheria kudhibiti michezo ya kulipwa

Bunge la Tanzania limepitisha mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) inayolitaka baraza hilo kuongezewa nguvu ya kusimamia michezo ya kulipwa kama inavyofanya kwenye michezo ya ridhaa.

Akiwasilisha muswada wa sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali namba tatu ya Mwaka 2018, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Aderadius Kilangi amesema marekebisho hayo yamelenga kuipa nguvu ya kisheria BMT ili kuweza kudhibiti michezo ya kulipwa.

Kilangi amesema vyama vingi vya michezo ya kulipwa vimekuwa vikikwepa kusajiliwa chini ya sheria ya baraza hilo kwa kisingizio kuwa tafsri ya michezo iliyoko kwenye sheria, inamaanisha michezo ya ridhaa na siyo michezo ya kulipwa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Uatawala Mohamed Mchengerwa amesema chini ya mabadiliko hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa na nguvu ya kisheria ya kuingilia kesi yoyote itakayofunguliwa na baraza hilo au dhidi ya baraza hilo.