Azam FC yazidi kuinyanyasa Yanga Kombe la Mapinduzi

|
Ni wakati Chirwa alipofunga alipofunga bao la tatu.

Azam FC, imefanya kweli baada ya kuichapa Yanga mabao 3-0 kwenye mchezo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi uliomalizika leo Jumamosi usiku.

Azam FC ilianza vyema mchezo huo, dakika ya kwanza ambapo mshambuliaji Obrey Chirwa, alikosa nafasi ya wazi baada ya kupokea pasi safi ya Enock Atta na kupiga shuti lililodakwa na kipa wa Yanga, Ibrahim Hamid.

Chirwa alirekebisha makosa yake dakika ya 33 na akiipatia Azam FC bao la uongozi akimalizia pande safi la kiungo mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu.

Winga Enock Atta, aliyekuwa akisheherekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa leo, aliimaliza siku yake vema kwa kuipatia bao la pili Azam FC dakika ya 44 kwa mpira wa moja kwa moja adhabu ndogo, iliyotokana na Kutinyu kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la 18.

Kipindi cha pili Azam FC iliendelea kulisakama lango la Yanga, ambapo ilifanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 60 lililofungwa na Chirwa, ambaye alikuwa akiiadhibu kwa mara ya pili timu yake hiyo ya zamani.

Huo ni ushindi mnono wa tatu kwa Azam FC kwenye michuano hiyo dhidi ya Yanga, mwaka 2012 iliichapa mabao 3-1 huku pia ikiwa na rekodi ya kuinyuka mabao 4-0, ambapo mara zote ilipopata ushindi iliweza kutwaa taji la michuano hiyo.

Kombe la Mapinduzi
Maoni