Chilunda apiga mabao manne akiipeleka Azam nusu fainali Kagame Cup

|
Shaaban Idd 'Chilunda' (kushoto) akikabidhiwa mpira baada ya kuifungia Azam FC mabao 4 kwenye mchezo wa robo fainali Kombe la Kagame dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda. Azam ilishinda mabao 4-2.

Mshambuliaji kinda wa Azam FC, Shaaban Idd ‘Chilunda’ amekuwa mchezaji wa kwanza kupiga ‘hat-trick’ kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mwaka huu alipoiongoza timu yake kuichapa Rayon Sports mabao 4-2.

Katika mchezo huo wa robo fainali uliopigwa jana kwenye dimba la Taifa, Dar es Salaam, Chilunda alifunga mabao yote manne, huku matatu akiyafunga ndani ya dakika 20, akifunga la kwanza katika dakika ya 19, la pili dakika ya 33 na la tatu dakika ya 39.

Kabla kipindi cha kwanza hakijamalizika, Rayon Sports walipata bao la kwanza kupitia kwa Rwatubyaye dakika ya 42.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kuendelea kutawala mchezo na kupata bao la nne katika dakika ya 64 huku Rayon nao wakiongeza ushindani na kupata bao la pili dakika ya 81 kupitia kwa Djabel.

Matokeo hayo sasa yatawakutanisha Azam FC ambao ndiyo mabingwa watetezi uso kwa uso na mabingwa wa Kenya, Gor Mahia katika mchezo wa nusu fainali utakaopigwa kesho kwenye dimba la Taifa Dar es Salaam.

CECAFA
Maoni