Chirwa: Natamani kuifunga Yanga iliyobaki Dar

|
Obrey Chirwa alipokuwa akishangilia bao lake dhidi ya Yanga.

Mshambuliaji wa Azam FC, Obrey Chirwa, ameweka wazi kuwa atafurahi zaidi atakapokifunga kikosi kamili cha Yanga kilichobakia jijini Dar es Salaam.

Kauli ya Chirwa imekuja muda mchache mara baada ya kufunga mabao mawili yaliyoiongoza Azam FC kuichapa Yanga mabao 3-0 juzi Jumamosi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, bao lingine kiliwekwa kimiani kwa mpira wa adhabu ndogo na Enock Atta.

Kwenye mchezo huo kikosi cha Yanga kilionekana kuwa wachezaji mchanganyiko baadhi kutoka timu kubwa na wengine wa timu yao ya vijana ‘Yanga U-20’.

“Mimi kila siku ninapofunga na kutoa pasi ya bao huwa najisikia raha tu, kwa sababu nafanya kazi na wenzangu, marafiki zangu, mimi siwezi kushinda peke yangu uwanjani, tunashinda kama timu na kupoteza kama timu, siwezi kucheza peke yangu uwanjani.

“Kwa mimi kwa uwezo wangu nataka niifunge timu ile iliyoko Dar es Salaam, nitajua na kufurahi kuwa nishaifunga Yanga,” alisema mshambuliaji huyo aliyeiteketeza timu yake hiyo ya zamani.

Kuelekea mechi mbili za mwisho za Kundi B la michuano hiyo dhidi ya KVZ na Malindi, alisema kuwa watahakikisha wanashinda mechi hizo, huku akigusia kuwa cha muhimu ni kufanya maandalizi vizuri wao kama wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

Aidha kwa kufunga mabao hayo, yamemfanya Chirwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania kuwa mfungaji wa michuano hiyo, akiwa na mabao mawili sawa na mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere.

Kombe la Mapinduzi
Maoni