Test
Yanga yavunja mwiko, yaichapa Mbao kwa mara ya kwanza Kirumba

Mabingwa wa Kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga SC leo wamevunja mwiko kwa kupata ushindi kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza dhidi ya Mbao FC.

Tangu Mbao ipande daraja haijawahi kupoteza wala kufungwa goli lolote na Yanga kwenye uwanja wake huo wa nyumbani, wakiwa wamekutana michezo mitatu na Yanga kufungwa katika michezo yote.

Katika mchezo wa leo Mbao walitangulia kupata bao dakika ya 45+2 kupitia kwa Ndaki Robert lakini Yanga wakarejea na nguvu mpya kipindi cha pili na kufunga goli la kusawazisha kupitia kwa Heritier Makambo dakika ya 50, kabla ya Amissi Tambwe kufunga bao la ushindi kwa penati baada ya beki wa Mbao kushika mpira ndani ya eneo la hatari. 

Matokeo ya mechi zote za leo ni haya hapa:- 

FT: Mbeya City 0-1 TZ Prisons (Salum Kimenya 70’)

FT: KMC 1-0 Mtibwa Sugar (Sadala Lipangile 2’)

FT: Ndanda SC 2-0 Singida United (Vitalis Mayanga 9’, Mohamed Mkopi 81’)

FT: Mbao FC 1-2 Yanga SC (Ndaki Robert 45’+2, Heritier Makambo 50’, Amissi Tambwe 68’p)

FT: Stand United 3-2 Lipuli FC (Mourice Mahela 33’, Datus Peter 59’, Jacob Masawe 90’+2 : Paul Nonga 28’, Jimmy Shoji 72’)

Makonda kuongoza kamati ya 'kuipeleka' Taifa Stars AFCON

Shirikisho la Soka Tanzania TFF imetangaza kamati ya watu 14 kwaajili ya kuisaidia Timu ya Taifa, (Taifa Stars) kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu zitakazofanyika nchini Misri.

Kazi kubwa ya kamati hiyo itakuwa ni kuhakikisha Taifa Stars inapata ushindi katika mchezo wa mwisho wa kuwania tiketi hiyo dhidi ya Uganda utakapigwa nchini mwezi Machi mwaka huu.

Kamati hiyo itaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda atakayekuwa Mwenyekiti, huku Katibu wake akiwa Mhandisi Hersi Said.

Wajumbe wa kamati hiyo ni Mohamed Dewji, Haji Manara, Jerry Muro, Farouk Barhoza, Salim Abdallah, Mohamed Nassor, Patrick Kahemele, Abdallah Bin Kleb, Tedy Mapunda, Philimon Ntaihaja, Farid Nahid na Faraji Asas.

Simba, Mwadui zaendeleza dozi ligi kuu, Azam yachechemea

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu Tanzania Bara Simba SC wamepata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Simba imepata mabao yake kupitia kwa John Bocco aliyefunga mawili dakika ya 28 kwa penati na dakika ya 46, huku bao lingine likifungwa na Adam Salamba dakika ya 45+2.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi 42 ikiendelea kubaki nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC wenye pointi 50 na kileleni bado yupo Yanga akiwa na pointi 58.

Kwa upande wao African Lyon wamesalia mkiani wakiwa na pointi 21 katika michezo 27 waliyocheza.

Katika mchezo mwingine, Azam FC imeendelea kuangusha pointi baada ya leo kubanwa na Coastal Union kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

Wenyeji Coastal Union ndiyo waliotangulia kupata bao dakika ya 45+2 kupitia kwa Ayoub Lyanga, lakini Obrey Chirwa akasawazisha bao hilo dakika ya 51 ya mchezo.  

Azam sasa wamefikisha pointi 50 katika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 24 huku Coastal wakiwa nafasi ya saba na pointi 34 baada ya kucheza michezo 26.

Nayo Mwadui FC imeendeleza wimbi lake la ushindi kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Mwadui Complex baada ya leo kuichapa Biashara United mabao 2-1.

Mwadui walianza kupata bao dakika ya 45 kwa tiki taka ya Salim Salim Aiyee na kisha Biashara kusawazisha dakika ya 51 kwa penati iliyopigwa na Wazir Rashid Jr kabla ya Salim Aiyee kufunga bao la ushindi dakika ya 64 akimalizia krosi ya Ditram Nchimbi.

Mwadui wamefikisha pointi 33 baada ya kuchezo mechi 28 na kukaa katika nafasi ya nane huku Biashara wakisalia katika nafasi yake ya 19 na pointi 23 katika michezo 26 waliyocheza.

Mchezo mwingine ulipigwa leo umeshuhudia Ruvu Shooting wakitoka suluhu na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Singida United yaikomalia Lipuli FC nyumbani kwao

Timu ya Lipuli FC imelazimika kutumia dakika za nyongeza kusawazisha bao ili kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo kwenye Dimba la Samora Mjini Iringa.

Wageni wa mchezo huo Singida United ndiyo waliotangulia kupata bao dakika ya 46 kupitia kwa Geofrey Mwashiuya kabla ya Lipuli kusawazisha dakika ya 61 kupitia kwa Haruna Shamte.

Singida walijipanga na kuongeza bao la pili dakika ya 84 kupitia kwa Boniphace Maganga lakini Miraji Athuman akaisawazisha Lipuli dakika ya 90+1 katika dakika tatu za nyongeza.

Matokeo hayo yameifanya kila timu iondoke na alama moja, Lipuli ikifikisha alama 38 katika nafasi ya nne huku Singiga ikifikisha alama 29 na kukaa nafasi ya 15.  

Simba yaitafuna Yanga kwa bao la Meddie Kagere

Wekundu wa Msimbazi Simba SC imewatetemesha watani wao wa jadi Yanga SC kwa kuipa kipigo cha bao 1-0 katika mchezo mkali uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Bao pekee la Simba limefungwa na Meddie Kagere dakika ya 71 kwa kichwa akimalizia krosi ya John Bocco na kuamsha shangwe za kutosha kwa mashabiki wa timu hiyo waliofurika ndani ya Dimba la Taifa.

Mara baada ya mchezo, kiungo wa Yanga Feisal Salum amesema Simba wamekuwa na bati kwenye huyo kwa kutumia nafasi waliyoipata na wao hawakati tamaa kwenye mbio zao za ubingwa wa ligi kuu msimu huu.

Kwa upande wake mfungaji wa bao pekee la Simba Meddie Kagere amesema tayari wameshayasahu matokeo hayo na sasa wanajipanga kwaajili ya mchezo ulio mbele yao huku akiwajibu wanaobeza umri wake akisema kuwa akili ya uwanjani ni muhimu kuliko umri.

Baada ya matokeo hayo Simba imefikisha pointi 39, ikiwa ni pointi 19 nyuma ya vinara Yanga huku Azam wakiwa nafasi ya pili na pointi 49.

Ligi hiyo itaendelea kesho Jumapili kwa mchezo mmoja kati ya Lipuli FC watakaokuwa nyumbani kuwakaribisha Singida United.

Waamuzi Yanga vs Simba wawekwa hadharani

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtangaza Hance Mabena kutoka Tanga (pichani) kuwa mwamuzi wa mchezo wa kesho wa #LigiKuuTanzaniaBara kati ya Yanga na Simba utakaopigwa kesho Februari 16, 2019 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mabena atakayesimama katikati, atasaidiwa na Mohamed Mkono kutoka Tanga pamoja na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam watakaosimama pembeni wakati Elly Sasii kutoka Dar es salaam atakuwa mwamuzi wa akiba.

Sakata la ‘Ninja’ wa Yanga lazidi kupigwa kalenda

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeridhia ombi la Yanga la kuahirisha kusikiliza shauri dhidi ya beki wake Abdallah Haji Shaibu ‘Ninja’ na imepanga kusikiliza shauri hilo katika kikao kijacho. 

Taarifa iliyotolewa leo na TFF imeeleza kuwa sababu ya kukubali ombi hilo ni kwasababu Shaibu alipata wito wa kamati hiyo wakati akiwa nje ya Dar es Salaam na kusisitiza kuwa katika kikao kijacho haitapokea tena udhuru wowote isipokuwa kama atakuwa katika majukumu ya timu ya Taifa. 

Taarifa hiyo ya TFF haijaweka bayana ni lini kikao hicho kijacho kitafanyika.

Shaibu alipelekwa kwenye kamati hiyo na Kamati ya Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union, katika mechi iliyozikutanisha timu hizo Februari 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.