Test
KMC yazidi kujisuka, yanasa kiungo kutoka Kenya

Timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) imeendelea kujipanga kwaajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kumsajili kiungo mshambuliaji, Abdul Hillary Hassan kutoka Tusker FC ya Kenya.

Afisa Habari wa KMC, Walter Harrison amesema mchezaji huyo ambaye ni Mtanzania, amejiunga rasmi na klabu ya KMC FC kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Kiungo huyo mshambuliaji mwenye umri wa miaka 23, urefu wa futi 6 na uwezo wa kutumia miguu yote kwa ufasaha, anakuwa mchezaji mpya wa tano kusajiliwa KMC baada ya kipa Juma Kaseja na mabeki Aaron Lulambo, Sadallah Lipangile na Ali Ali. 

Kombe la Kagame kufanyiwa mageuzi makubwa

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepanga kuongeza timu shiriki katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) msimu ujao na kufikia timu 16.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye amesema timu hizo 16 zitakuwa katika makundi manne.

Sanjari na hilo Musonye amesema CECAFA inatarajia kubadili kalenda yake ya mashindano ili kufuata ratiba ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) na kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Aidha Musonye amesema kuna uwezekano mkubwa wa nchi za Malawi, Zambia na Congo DR kujiunga na CECAFA baada ya mataifa hayo kuomba kuandaa fainali za Kombe la Kagame msimu ujao wa 2018/2019.

Netiboli Tanzania yatolewa kifungoni

Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kimefunguliwa na Chama cha Netiboli cha Kimataifa (FINA) na sasa kitakuwa huru kushiriki michuano ya kimataifa kwa klabu na timu za taifa.

Kufunguliwa huko kwa CHANETA kumekuja baada ya kukubaliwa ombi lao na FINA huku wakitakiwa kulipa ada ya malimbikizo ya uanachama ya miaka mitatu ambayo kila mwaka hugharimu kiasi cha dola 1,500 za Marekani.

Mwenyekiti wa CHANETA, Dkt. Devota Marwa amesema watalipa ada hiyo wakati wa mashindano ya kufuzu kwa michuano ya Afrika itakayofanyika nchini Zambia mwezi ujao ila Tanzania haitapeleka timu msimu huu.

Feisal Salum atua rasmi Singida United

Klabu ya Singida United imefanikiwa kuinasa saini ya mchezaji, Feisal Salum Abdallah ‘FEI TOTO’ kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea JKU ya Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa leo, Alhamisi na Singida United imeeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo umekubaliana na uongozi wa JKU kuhusu ada ya uhamisho ambapo Singida United wamekubali kulipa gharama za kufidia miaka miwili ya mkataba ambao mchezaji huyo alikuwa ameubakiza katika klabu ya JKU.

Huu ni mwendelezo wa kukisuka kikosi cha timu hiyo chini ya kocha Hemedi Selemani Morocco wakiwa tayari wamewasajili Habib Kiyombo kutoka Mbao FC, Tibar George kutoka Ndanda FC, Eliuter Mpepo kutoka Tanzania Prisons na David Kisu kutoka Njombe Mji.

Croatia yaweka historia Kombe la Dunia ikiifuata Ufaransa fainali

Timu ya Taifa ya Croatia imeweka historia kwenye michuano ya Kombe la Dunia baada ya kufanikiwa kuingia fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yake ya soka.

Croatia wameandika historia hiyo baada ya kuichapa England mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali ya pili uliopigwa usiku wa jana kwenye dimba la Luzhniki jijini Moscow, nchini Urusi.

Katika mchezo huo uliopigwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1, England ndiyo walioanza kujipatia bao kwa mpira wa adhabu ndogo nje kidogo ya 18 kupitia kwa Kieran Trippier dakika ya 5.

Kipindi cha pili, Croatia walipambana na kurejea mchezoni huku wakitawala zaidi mchezo na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 68 kupitia kwa Ivan Perisic, matokeo yaliyodumu kwa dakika zote 90.

Katika dakika 30 za ziada, Croatia walimaliza kazi kwa kufunga bao la pili kupitia kwa mkongwe Mario Mandzukic dakika ya 109, na kuisukuma rasmi England nje ya mashindano hayo.

Croatia imekuwa ni timu ya kwanza kwenye histori ya michuano hiyo kuondoka na ushindi licha ya kutanguliwa kufungwa kwenye michezo yote mitatu ya hatua za mtoano, ikiwa imeitoa Denmark kwenye hatua ya 16 bora kwa mikwaju ya penati, ikaitoa Urusi kwenye robo fainali pia kwa mikwaju ya penati kabla ya kuitupa nje England kwenye nusu fainali, mechi zote zikichezwa kwa dakika 120.

Croatia pia imekuwa ni timu ya 13 kwenye historia ya mashindano ya Kombe la Dunia kutinga hatua ya fainali kwa mara ya kwanza na sasa itakutana na Ufaransa katika mchezo wa fainali utakaopigwa Jumapili Julai 15 katika jiji la Moscow.

Ikumbukwe kuwa nafasi bora zaidi ambayo Croatia imewahi kufika ni hatua ya nusu fainali wakati wa fainali za michuano hiyo za mwaka 1998 walipofungwa na Ufaransa ambao ndiyo waliokuwa mabingwa wa kombe hilo.

Katika mashindano ya mwaka huu, Ufaransa wametinga hatua hiyo ya fainali baada ya kuitoa Ubelgiji kwa kuichapa bao 1-0 kwenye nusu fainali na sasa Ubelgiji watacheza na England kwenye mchezo wa kusaka mshindi wa tatu utakaopigwa Jumamosi, Julai 14 katika mji wa St. Petersburg.

Ni Simba na Azam fainali Kombe la Kagame

Wababe wa soka nchini Tanzania Simba SC na Azam FC ndiyo watakaokutana kwenye mchezo wa fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

Fainali hiyo ya kukata na shoka itapigwa Ijumaa wiki hii kwenye dimba la Taifa Jijini Dar es Salaam na kukufikia mbashara kupitia Azam Sports 2.

Simba imefikia hatua hiyo baada ya jana kuichapa JKU bao 1-0, kwenye nusu fainali ya pili, bao pekee la ushindi likifungwa na mshambuliaji wake mpya Meddie Kagere dakika ya 44 akimalizia pasi ya Nicholas Gyan.

Kwa upande wa Azam, wao wamewachapa mabingwa wa Kenya, Gor Mahia mabao 2-0 kwenye nusu fainali ya kwanza iliyopigwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 kumalizika bila timu hizo kufungana.

Mabao ya Azam yamefungwa na Ditram Nchimbi dakika ya 92 huku Bruce Kangwa akipachika bao la pili dakika ya 100.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa wababe hawa kukutana kwenye michuano hiyo huku Azam FC wakisaka heshima ya kulitetea taji hilo ambalo walilitwaa kwa mara ya kwanza mwaka 2015.

Mchezo wa fainali utakaopigwa saa 10:00 jioni utatanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, kati ya Gor Mahia ya Kenya na JKU ya Zanzibar.

Nusu fainali Kombe la Kagame kupigwa leo

Mechi mbili za nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) zinapigwa leo kwenye Dimba la Taifa, jijini Dar es Salaam, zote zikikufikia mbashara kupitia Azam Sports 2.

Nusu fainal ya kwanza itapigwa saa 8:00 mchana na itakuwa ni kati ya mabingwa watetezi Azam FC dhidi ya mabingwa Kenya, Gor Mahia.

Azam wamefikia hatua hiyo baada ya kuwatupa nje Rayon Sports ya Rwanda kwa kuishushia kipigo cha mabao 4-2 huku Gor Mahia ikiichapa Vipers ya Uganda mabao 2 -1.

Nusu fainali ya pili itawakutanisha mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC dhidi ya mabingwa wa Zanzibar, JKU, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 11:00 jioni.

Simba ambao ndiyo mabingwa wa kihistoria wa kombe hilo, wamefikia hatua hiyo baada ya kuitoa AS Port ya Djibout kwa kuichapa bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali huku JKU ikiitoa Singida United kwa penati 4-3.