Test
Simba yatangaza viingilio mechi yake na TP Mazembe

Klabu ya Simba imetangaza viingilio katika mchezo wao war obo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa Jumamosi Aprili 6, kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Akitaja viingilio hivyo leo, Msemaji wa Simba Haji Manara amesema kiingilio cha chini kitakuwa ni shilingi 4,000 (Mzunguko) kwa watakaonunu tiketi mapema kuanzia leo Aprili 2, hadi Ijumaa saa 6:00 usiku na Jumamosi itakuwa sh 5,000.

Viingilio vingine ni shilingi 10,000 kwa VIP A, shilingi 20,000 kwa VIP B, na shilingi 100,000 kwa tiketi za Platinum.

Manara amesema kauli mbiu itakayotumika kwenye mchezo huo ni ‘YES WE CAN” na kueleza sababu ya kutumia kaulimbiu hiyo.

“Tunakwenda na Slogan ile ile ya Yes We Can, kwakuwa imelipa na inatuweka salama zaidi huku tukicheza bila presha!! Tutawakabili Mazembe huku tukiujua ubora wao lakini Simba ishazoea kuishangaza Afrika na dunia kwa ujumla na tutafanya hvyo Jumamosi Insha'Allah”, amesema Manara. 

Nyota 20 Yanga waifuata Ndanda bila Ajibu

Jumla  ya nyota 20 wa kikosi cha mabingwa wa kihistoria  nchini, Yanga SC, leo alfajiri wameanza safari kueleka Mtwara tayari kwa mchezo wa ligi dhidi ya wenyeji wao Ndanda FC.

Mchezo huo umepangwa kutimua vumbi Aprili 4 kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona na utakuwa mbashara Azam Sports 2 kuanzia saa 10:00 jioni.

Afisa Habari wa timu hiyo Dismas Ten amesema kuwa nahodha wao Ibrahim Ajib ataendelea kukosekana kikosini kupisha majeraha madogo aliyo nayo huku Juma Abdul akirejea kikosini baada ya kupona majeraha yake.

"Ibrahim Ajib bado tutaendelea kumkosa kikosini kutokana na majeraha ya mguu, lakini jambo jema ni kwamba Juma Abdul amerejea kikosini na atakuwa sehemu ya msafara wa kikosi chetu, mchezo utakuwa mgumu lakini maandalizi tuliyoyafanya yanatosha kutupa matokeo mazuri".

Simba yalipa kisasi kwa Mbao FC

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC walipa kisasi kwa Mbao FC kwa kuichapa mabao 3-0 katika mchezo wa kiporo wa ligi hiyo uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mabao ya Simba yametiwa kimiani na John Bocco aliyefunga mawili dakika ya 25 na 59 kwa penati baada ya Peter Mwangosi kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Bao la tatu limefungwa na Meddie Kagere kwa penati pia baada yay eye mwenyewe kuangushwa ndani ya eneo la hatari dakika ya 80. Matokeo hayo ni kisasi cha mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. 

Ushindi huo unawapa Simba alama tatu muhimu na kufikisha alama 57 katika nafasi yake ya tatu nyuma ya Azam FC wenye alama 59 na Yanga wakiwa kileleni na pointi zao 67. 

Yanga yaipiga Alliance na kutinga nusu fainali ASFC

Yanga SC imekuwa timu ya mwisho kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) baada ya kuitupa nje Alliance FC ya jijini Mwanza kwa mikwaju ya penati 4-3 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Yanga ndiyo waliotangulia kupata bao kupitia kwa Heritier Makambo dakika ya 38 akimalizia pasi ya Pius Buswita, lakini Alliance wakasawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Joseph James akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Godlove Mdumule dakika ya 62.  

Baada ya dakika 90, ikapigwa mikwaju ya penati ambapo kati ya penati sita kwa kila timu, Yanga ilipata penati mbili huku Alliance wakifunga penati tatu.

Waliofunga penati kwa upande wa Yanga ni Paul Godfrey, Thabani Kamusoko, Haruna Moshi na Deusi Kaseke huku Kelvin Yondan na Mrisho Ngassa wakikosa penati zao.

Kwa upande wa Alliance, waliofunga penati ni James Joseph, Geofrey Luseke na Sameer Vicent huku Martin Kiggi, Dickson Ambundo na Siraji Juma wakikosa penati zao na kipa wa Yanga Klaus Kindoki kuibuka shujaa kwa kuokoa penati mbili ikiwemo ya mwisho iliyowapa ushindi.

Yanga sasa itacheza na Lipuli FC kwenye hatua ya nusu fainali huku Azam FC wakiwa wenyeji wa KMC FC.

Twiga Stars yawatoa hofu Watanzania kuelekea mchezo dhidi ya DRC

Timu ya taifa ya Tanzania ya wanawake Twiga Stars, wamewataoa hofu Watanzania kuelekea kwenye mchezo wao wa April 5, mwaka huu dhidi ya DR.Congo ikiwa ni mchezo wa kuwania kufuzu Olimpiki,mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha Msaidizi wa Twiga Stars, Edna Lema amesema kikosi chake kipo katika mazoezi makali kuelekea mchezo huo utakaochezwa wiki ijayo na marudiano yake yatafanyika Aprili 9 mwaka huu huko DR Congo.

Azam yaichapa Kagera Sugar na kutinga nusu fainali ASFC

Kiungo Joseph Mahundi ameifungia Azam FC bao pekee la ushindi dakika ya 80 katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Katika mchezo, Azam walipata pigo baada ya golikipa wake Razak Abarola kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 68 baada ya kumchezea vibaya mchezaji wa Kagera Sugar nje kidogo ya 18 akiwa katika nafasi ya kufunga.

Ushindi huo wa bao 1-0 unaipeleka Azam FC nusu fainali ambako itakutana na KMC.

JKT Tanzania yatambulisha kocha mpya

Uongozi wa timu ya soka ya JKT Tanzania umemtangaza Abdallah Mohamedi Baresi kuwa kocha mkuu wa kikosi chake baada ya kumsimamisha kazi Bakari Shime.

Baresi ndiye aliyetwaa tuzo ya Kocha Bora wa #LigiKuuTanzaniaBara kwa msimu uliopita alipokuwa akiifundisha Tanzania Prisons iliyomaliza msimu ikiwa nafasi ya nne kabla ya kutimuliwa katikati ya msimu huu kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo.

Afisa Habari wa timu hiyo Koplo Jamila Mutabazi amesema Baresi ameshaanza kazi mara moja baada ya kutangazwa kwake.