Mechi Nane kuendeleza raha za VPL kuanzia Jumamosi hii

|
Kikosi kazi cha Azam TV tayari kimewasili mkoani Iringa kukuletea matangazo ya moja kwa moja ya mchezo kati ya Lipuli FC vs Mtibwa Sugar

Kimbembe cha Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) kinaendelea kuanzia kesho Jumamosi (Januari 13, 2018) kwa mechi nane za raundi ya 13 kupigwa katika viwanja nane tofauti.

Mechi tatu kati ya nane zinafungua raundi hiyo Jumamosi ambapo Lipuli FC itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika dimba la Samora mjini Iringa, wakati Stand United watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting katika dimba la Kambarage mjini Shinyanga.

Mbao FC waliotoka kuipiga Yanga 2-0 katika dimba la CCM Kirumba kesho watasafiri hadi mkoani Mtwara kuwafuata Ndanda FC, mchezo utakaopigwa katika dimba la Nangwanda Sijaona.

Jumapili kutakuwa na patashika ya ‘Mbeya Derby’, pale ndugu wawili wa jiji la Mbeya, Tanzania Prisons na Mbeya City watakapoumana katika dimba la Sokoine jijini Mbeya.

Ligi hiyo itaendelea Jumatatu kwa mchezo mmoja katika dimba la Sabasaba mjini Njombe, ambapo Njombe Mji watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar.

Mabingwa watetezi Yanga, watashuka dimbani siku ya Jumatano, Januari 17 katika dimba la Uhuru Dar es Salaam kuwavaa wachimba madini wa Mwadui FC.

Alhamisi, Januauri 18 ni vinara wa ligi hiyo, Simba SC watakaoshuka katika dimba la Uhuru Dar es Salaam kuvaana na matajiri wa Singida United, wakati Azam FC wakiwa ni wenyeji wa Majimaji FC mjini Songea siku hiyo hiyo.

Mechi zote hizo utazishuhudia LIVE kupitia Azam TV.

VPL
Maoni