Modric amfunika Ronaldo kwa mara nyingine

|
Luka Modric amekuwa raia wa kwanza wa Croatia kushinda tuzo ya mchezaji bora wa FIFA.

Kiungo wa kimataifa wa Croatia Luka Modric amewashinda Cristiano Ronaldo na Mohamed Salah na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa FIFA.

Modric ameshinda tuzo hiyo kufuatia kuwa na msimu wenye mafanikio makubwa akiwa na Real Madrid kwa kuisaidia miamba hiyo ya Hispania kutwaa ubngwa wa tatu mfululizo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).

Mchango wake pia katika kombe la dunia umepongezwa kwa kuiongoza timu ya Croatia kucheza fainali ya kombe hilo kwa mara ya kwanza na licha ya kufungwa na Ufaransa lakini Modric alitwaa tuzo ya Golden Ball.

Hata hivyo sherehe hizo ziliingia doa baada ya Ronaldo aliyekuwa akitajwa sana kustahili tuzo hiyo kwa kushinda taji la tano la UCL kutooneka kwenye ukumbi wakati wa utoaji wa tuzo hizo kutokana na kubanwa na ratiba za katikati ya wiki zinazoikabili timu yake ya Juventus.

Baada ya kupokea tuzo hiyo, Modric alitoa heshima kwa aliyekuwa nahodha wa taifa hilo kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1998, Zvonimir Boban, aliyemtaja kuwa shujaa wake.

"Ndiye aliyenihamaisha sana na kikosi chao ndicho kilichotupa Imani kuwa tunaweza kufanikiwa kushinda kitu kikubwa nchini Urusi. Ni matumaini yangu tutakuwa hivyo kwa vizazi vijavyo” alisema Modric.

"Tuzo hii inadhihirisha sote tunaweza kuwa chochote tutakacho tukifanya juhudi, tukijitoa na tukiamini. Ndoto zote hutimia”

Mshambuliaji wa Misri, Mohamed Salah alifanikiwa kutwaa tuzo ya goli bora zaidi kutokana na goli aliloifungia timu yake ya Liverpool dhidi ya wapinzani wao wa jadi Everton.

Kipa wa zamani wa Chelsea aliyehamia Real Madrid, Thibaut Courtois alishinda tuzo ya golikipa bora kutokana na kiwango alichokionyesha wakati wa kombe la dunia huku tuzo ya kocha bora ikitwaliwa na Didier Deschamps wa Ufaransa aliyeliongoza taifa hilo kutwaa ubingwa kwa kuifunga Croatia.

Soka
Maoni