Obrey Chirwa atua rasmi Azam FC

|
Mshambuliaji Obrey Chirwa alipotambulishwa rasmi na klabu ya Azam FC leo.

Aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga msimu uliopita kabla ya kutimkia nchini Misri, Obrey Chirwa, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na Azam FC.

Chirwa raia wa Zambia ametambulishwa rasmi leo, Novemba 08 mbele ya wanahabari na kukabidhiwa jezi namba saba (7), ambayo ilikuwa ikitumiwa na mshambuliaji Wazir Junior ambaye uongozi wa Azam haujaweka wazi endapo utaachana naye au la.

Chirwa ameitumikia Yanga kwa takriban misimu miwili na mkataba wake ulipomalizika mwezi Juni mwaka huu aliachana na Yanga na kujiunga na Nogoom FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Misri ambayo ameitumikia kwa kipindi kisichozidi miezi minne.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zimeeleza kuwa mchezaji huyo ameamua kuvunja mkataba na timu hiyo ya Misri baada ya kushindwa kumlipa stahiki zake na aliamua kurejea nchini Tanzania kwa lengo la kujiunga na Yanga.

Wakati taratibu za uongozi wa Yanga kumsajili tena Chirwa, kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alinukuliwa akisema kuwa hamuhitaji mchezaji huyo, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa mchezaji huyo alitaka kulipwa pesa nyingi kuliko kiwango ambacho Yanga ilimuandalia na ndipo Azam wakaamua kuingia katika makubaliano naye.

Katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Chirwa aliifungia Yanga mabao 12 akishika nafasi ya nne katika orodha ya wafungaji bora akiwa ndiye kinara wa mabao ndani ya klabu hiyo.

Usajili
Maoni