Samatta aing'arisha Genk,mechi ya kufuzu Europa League

|
Mbwana Samatta alionekana kuwa mwenye furaha zaidi baada ya kufunga bao hilo.

Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta jana ameifungia bao la pili la timu yake, KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Lech Poznan ya Poland katika mchezo wa kwanza wa raundi ya tatu ya mchujo michuano ya UEFA Europa League.

Samatta alifunga bao hilo dakika ya 56, baada ya kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy kutangulia kufunga la kwanza dakika ya 44, katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Luminus Arena mjini Genk.

Mshambuliaji huyo ambaye yupo kwenye mawindo ya kusajiliwa na vilabu kadhaa barani Ulaya,  alionekana kuwa mwenye furaha zaidi baada ya kufunga bao hilo na kupitia ukurasa wake wa Instagram aliweka ujumbe uliosemeka "Haina Kufeli".

Kwa matokeo hayo Genk watahitaji kwenda kuulinda ushindi wao katika mchezo wa marudiano Agosti 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa INEA mjini Poznan ili kwenda katika mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi, ambako watacheza mechi moja zaidi nyumbani na ugenini.

Soka
Maoni