Serengeti Boys yatwaa kombe nchini Rwanda

|
Serengeti Boys wakiwa na kombe lao la ubingwa wa mashindano maalum nchini Rwanda.

Timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 Serengeti Boys imeendelea kuwa na mfululizo wa kupata matokeo mazuri na mafanikio kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa wanayoshiriki baada ya Aprili 4 mwaka huu kuongeza taji lingine la ubingwa.

Katika mashindano maalum ya siku chache yaliyoandaliwa na shirikisho la soka la Rwanda (FERWAFA) imeshuhudiwa kwa mara nyingine tena Serengeti Boys ikimaliza mashindano hayo kama bingwa wake.

Licha ya sare ya mabao 3-3 na wenyeji Rwanda katika mchezo wa mwisho, Serengeti Boys ameshinda taji hilo baada ya kufikisha alama 4 zitokazonazo na ushindi wa 2-1 dhidi ya wanafainali wenza wa AFCON timu ya Cameroon pamoja na sare hiyo dhidi ya Rwanda.

 

Kwenye mchezo huu Rwanda ndiyo waliotangulia kupata mabao mawili ndani ya dakika 20 za kwanza, lakini Serengeti Boys wakatulia na kujibu mapigo, wakianza kufunga bao la kwanza dakika ya 30 kupitia kwa Edmund John, kisha Edmund John tena akaisawazishia Serengeti dakika ya 49 kabla ya Edson Mshirakandi kuifungia Tanzania bao la tatu dakika ya 83.

Cameroon wao wamemaliza wa pili na alama zao tatu walizozipata kufuatia ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji Rwanda na wakipoteza mechi yao ya pili dhidi ya Serengeti Boys.

Wenyeji Rwanda walioanza kwa kipigo wamefanikiwa kuvuna alama moja pekee baada ya kuisawazishia Serengeti Boys dakika za mwishoni hii leo.

Rasmi mashindano hayo ya mechi mbili mbili yamemalizika ambapo Serengeti Boys na Cameroon zinataraji kuja katika ardhi ya Tanzania tayari kwaajili ya fainali za AFCON kwa vijana zitakazoanza April 14 mwaka huu.

Soka
Maoni