Serikali yatoa msimamo idadi ya wachezaji wa kigeni

|
Dkt. Harrison Mwakyembe

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema idadi ya wachezaji saba wa kigeni katika timu za soka za Ligi Kuu Tanzania Bara inatosha kwa sasa na hakuna sababu yoyote ya kuiongeza au kuipunguza.

Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa msimamo huo leo, Jumanne  Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilolo mkoani Iringa Venance Mwamoto, aliyehoji ni kwanini wachezaji wa kigeni wasizuiliwe au idadi yao kupunguzwa kwa lengo la kuboresha timu ya taifa.

Dkt. Mwakyembe amesema idadi hiyo ilipendekezwa na wadau husika zikiwemo timu zenyewe na kwamba hadi sasa idadi hiyo haijaathiri ubora wa timu ya taifa zaidi ya kuwa na faida kwenye soka la Tanzania kwa kuwa hadi sasa katika timu zote 16 za ligi kuu, wachezaji wa kigeni waliopo ni 35 pekee ambao ni sawa na asilimia 7 ya wachezaji wote wa timu hizo.

Akitaja manufaa ya uwepo wa wachezaji wa kigeni nchini, Dkt. Mwakyembe amesema wachezaji hao wanasaidia kuongeza ushindani katika ligi, kuwa fundisho kwa wachezaji wa ndani pamoja na kuitangaza Tanzania katika mataifa mengine kwa kuwa wachezaji hao hufuatiliwa kwa ukaribu na mataifa yao.

Kuhusu Serengeti Boys, Mwakyembe amesema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuisadia timu hiyo iliyoshiriki AFCON kwa vijana nchin Gabon kwa kuwa ndiyo inayotegemewa kuiwakilisha Tanzania katika Olimpiki ya mwaka 2020.

Soka
Maoni