Simba yailaza KMKM, yatinga nusu fainali Mapinduzi Cup

|
Mchezo huo uliambatana na burudani mbalimbali kutoka kwa kiungo wa Simba Clatous Chama ambaye aliamua kupiga danadana ndani ya mechi wakati Simba ikiongoza kwa bao 1-0.

Timu ya Simba imeibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya KMKM katika mchezo mgumu wa Kombe la Mapinduzi uliopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Bao la Simba lilifungwa na Rashid Juma dakika ya 83 ya mchezo akimalizia kwa kichwa mpira uliotemwa na kipa wa KMKM baada ya shuti la Clatous Chama.

Licha ya Simba kuanzisha kikosi chake kamili, ilikumbana na ugumu kwenye mchezo hasa kutokana na mbinu ya kujilinda iliyokuwa ikitumiwa na KMKM.

Mchezo huo uliambatana na vionjo mbalimbali ikiwemo pasi lukuki zilizokuwa zikipigwa na Simba hasa baada ya kupata bao, pamoja na vionjo vya danadana katikati ya mechi kutoka kwa kiungo Mzambia wa Simba, Clatous Chama.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi sita na hivyo kuwa ya kwanza kutinga hatua ya nusu fainali.

Katika mchezo mwingine goli la dakika ya mwisho kabisa ya mchezo lililofungwa na Haji Mwambe limeipa timu ya Jamhuri ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KVZ.

Michuano hiyo inaendelea leo kwa Azam FC kuminyana na KVZ saa 10:15 jioni huku Yanga ikicheza dhidi ya Malindi saa 2:15 usiku, mechi zote ukizipata LIVE Azam Sports 2.

Kombe la Mapinduzi
Maoni