Usain Bolt aachana na soka, ahamia kwenye biashara

|
Usain Bolt.

Mfalme wa mbio fupi duniani, Usain Bolt amethibitisha rasmi kuachana na michezo yote ikiwemo soka na sasa ameamua kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa ulimwenguni.

Mshindi huyo mara nane wa medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki, amesema maisha ya kiuanamichezo yamefikia tamati kwa upande wake hivyo ameamua kujikita katika miradi mingine.

Bolt mwenye umri wa miaka 32 amekuwa akijifua katika Klabu ya Central Coast Mariners kwa kipindi cha miezi miwili mwaka 2018.

Hata hivyo, Mjamaica huyo alilazimika kuachana na Mariners mwezi Oktoba baada ya uongozi wa klabu kushindwa kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kuingia naye mkataba wa ajira kama mchezaji rasmi wa kandanda.

Baada ya kustaafu riadha mwaka 2017, Usain Bolt alihakikisha anatimiza ndoto yake ya kuwa mchezaji soka na amefanikiwa kuacha kumbukumbu ya kuwahi kuzifumania nyavu mara mbili katika mechi mbili za kirafiki alizoichezea Mariners.

Soka
Maoni