Test
Vilabu 29 kuwania ubingwa wa Afrika Kanda ya Tano, Dar es Salaam

Zaidi ya klabu bingwa 29 za mchezo wa mpira wa kikapu kutoka nchi wanachama wa kanda ya tano ya Afrika zimethibitisha kushiriki michuano ya klabu bingwa ya Afrika kanda ya tano itakayofanyika nchini kuanzia Septemba 30 mwaka huu.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Pharess Magesa, amasema maandalizi ya michuano hiyo itakayofanyika uwanja wa ndani wa taifa jijini Dar es Salaam yamekamilika.

Magesa pia amewaomba wadau kuchangia kwa hali na mali ili mafanikio yapatikane na malengo yaliyokusudiwa yafikiwe.

Mtibwa kuilipa Santos kwa awamu tatu

Mkurugenzi wa Mtibwa Sugar Jamal Bayser amesema uongozi wa timu hiyo umefikia makubaliano ya jinsi ya kulipa fidia kwa klabu ya Santos ya Afrika Kusini ili iweze kuruhusiwa na Shirikiso la Soka Barani Afrika (CAF), kushiriki michuano ya Kimataifa

Akizungumza na Azam TV mara baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii ambao umemalizika kwa Mtibwa kufungwa mabao 2-1 na Simba, Bayser amesema watailipa fidia hiyo kwa awamu tatu na awamu ya kwanza ni sasa, huku akisisiza kuwa hakuna kikwazo chochote kwa wao kushiriki michuano hiyo.

Mtibwa ndiyo wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho lakini imetakiwa kumaliza deni hilo ili itolewe kifungoni.

Timu hiyo ilifungiwa na CAF baada ya kushindwa kwenda kwenye mchezo wa marudiano wa michuano ya CAF dhidi ya Santos mwaka 2003.

USM Alger yaitangulia Yanga Dar, yatamba kushinda

Wapinzani wa Yanga katika mchezo wa Kundi D wa Kombe la Shirikisho Afrika USM Alger wamewasili leo Jijini Dar es Salaam tayari kwa mchezo huo utakaochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa na kukufikia LIVE kupitia ZBC 2.

Katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, kocha msaidizi wa timu hiyo Rahim Azzedine amesema mchezo huo ni muhimu kwao na licha ya Yanga kuwa na timu bora, watapambana kupata ushindi ili iwarahisishie kazi mbele ya safari.

Wakati huo huo uongozi wa timu ya soka ya Yanga umesema kikosi chake kitarejea jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa tayari kwa mchezo huo ambao pia utatumika kumuaga nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub Ali ambaye sasa anakuwa meneja wa Yanga.

Ethiopia, Sudan Kusini zang'ara michuano ya kufuzu AFCON U17

Michuano ya CECAFA chini ya miaka 17 kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani hapa nchini, imeendela tena leo kwa michezo miwili kupigwa kwenye dimba la Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa kwanza umeshuhudia timu ya Sudan Kusini ikiichapa Djibout mabao 2-1 ambapo magoli ya Sudan Kusini yamefungwa na Deng Joseph dakika ya 5, na Victor Charles dakika ya 26 huku bao pekee la Djibout likifungwa na Remi Ahmed dakika ya 64.

Djibout walipoteza nafasi muhimu ya kusawazisha baada ya kukosa mkwaju wa penati walioipata dakika ya 88 ya mchezo.

Katika mchezo wa pili Ethiopia imeichapa Uganda bao 1-0, bao pekee la Ethiopia likifungwa na Mintesnot Wakjira dakika ya 13.

Michuano hiyo itaendelea kesho JUmatatu kwa mechi mbili kupigwa, ambapo Sudan itacheza na Somalia saa 8 mchana huku Burundi ikicheza na Rwanda saa 11 jioni.

Canavaro astaafu rasmi kucheza soka, jezi yake ampa Ninja

Baada ya utumishi uliotukuka wa zaidi ya miaka 10, nahodha wa mabingwa wa kihistoria wa Yanga, Nadir Haroub Ally Upapa maarufu kama Canavaro amestaafu rasmi kuitumikia klabu hiyo kama mchezaji na kuanza majukumu yake mapya kama meneja.

Katika tukio hilo, Yanga imecheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya  Mawenzi Market uliomalizika kwa Yanga kushinda bao 1-0, bao pekee likifungwa na mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Heritier Makambo.

 Canavaro ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kwenye mchezo wa leo, alicheza kwa takriban dakika 10 kisha likafanyika tukio la kumuaga rasmi, ambapo aligoma jezi yake nambari 23 isistaafishwe kama ilivyokuwa imeamriwa na uongozi wa timu hiyo.

Akieleza sababu za uamuzi huo, nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars, amesema hakufurahishwa na wazo la klabu kuistaafisha namba ya jezi yake aliyokuwa akiivaa kwani anaamini yupo mtu anaweza kuitendea haki jezi zaidi ya alivyofanya yeye na mtu huyo ni Abdallah Shaibu ‘Ninja’, ambaye alimkabidhi jezi hiyo hapo hapo dimbani.

 Pia Canavaro amemkabidhi kitambaa cha unahodha, pacha wake wa muda mrefu katika ulinzi, Kelvin Yondan.

Katika tukio hilo, Canavaro ametunukiwa tuzo mbili za heshima, moja ikiwa ni ya kudumu klabuni muda mrefu nay a pili ikiwa ni ya kuwa mchezaji pekee mwenye mataji mengi zaidi akiwa na Yanga.

Baada ya mchezo huo, Canavaro amezungumza na Azam TV ambapo amewataka wachezaji chipukizi waige mfano wake hasa katika suala la nidhamu, huku akiweka wazi kuwa waliompa nafasi ya Umeneja kwenye klabu yake ni wachezaji na siyo viongozi.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Yanga Dismas Ten, timu hiyo imepanga kuutumia mchezo wake wa Agosti 19 dhidi ya USM Alger kwenye dimba la Taifa Dar es Salaam kwaajili ya mashabiki wa Dar es Salaam kumuaga nyota huyo.

Kambi ya Yanga yazidi ‘kunoga’ Morogoro

Kambi ya Yanga inandelea vyema mkoani Morogoro tayari kwa kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu soka ya Tanzania Bara ambapo kwa kuanzia Agosti 12 mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mawenzi Market.

Yanga iliingia kambini wiki iliyopita ikiwa na wachezaji wake wapya waliosajiliwa na wale wa zamani ambapo kati ya wachezaji wapya waliopo kambini ni Feisal Salum aliyesajiliwa kutoka JKU ya Zanzibar.

Mwingine ni Mrisho Ngassa aliyerejea Yanga kwa mara ya pili akitokea Ndanda FC ya mkoani Mtwara.

Yanga ipo chini ya makocha Mwinyi Zahera raia wa Ufaransa mwenye asili ya DR Congo ambaye anasaidiwa na Noel Mwandila raia wa Zambia.

Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara watacheza mechi hiyo kirafiki Jumapili kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambayo pia itatumika kumuaga nahodha wake Nadir Haroub ambaye sasa anakuwa meneja wa timu hiyo.  

Mtibwa yajivunia kuwarejesha kundini nyota wake wa zamani

Mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), Klabu ya Mtibwa Sugar wamesema wana imani na usajili wao walioufanya hivi karibuni utawasaidia katika kufanya vizuri msimu ujao huku wakijivunia kurejea kwa wachezaji ambao wamewahi kuitumikia kwa mafanikio miaka ya nyuma.

Kocha wa timu hiyo, Zubeir Katwila amesema wachezaji wengi waliowasajili ni wale ambao wamewahi kuitumikia timu hiyo, hivyo anawafahamu vizuri na ana uhakika watamletea mafanikio msimu huu.

Akiwataja baadhi ya wachezaji ambao wamerejea baada ya kuondoka kwenye timu hiyo na kwenda vilabu vingine, Katwila amesema imemsajili Juma Luizio ambaye aliondoka Mtibwa kwenda nje ya nchi kabla ya kurejea nchini na kujiunga na Simba, lakini sasa amerejea kwenye timu yake hiyo ya zamani.

Mbali na Luizio, wengine ni mshambuliaji mwingine Jaffary Kibaya ambaye alikuwa Kagera Sugar, beki Ally Shomary kutoka Simba na kiungo Awadhi Juma ambaye alipoondoka Mtibwa alikwenda Simba kisha kuichezea Mwadui FC na sasa anarejea Mtibwa.

Katwila amesema timu hiyo haikuwa na nafasi nyingi za kujaza kulingana na mahitaji ya timu, hivyo wamesajili wachezaji wapya wasiozidi wanne, huku wengine wakiwa wamewachukua kwa mkopo kutoka timu mbalimbali.

Mtibwa Sugar itakuwa na kibarua mbele ya Simba, Agosti 18, mwaka huu katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kwenye dimba la CCM Kirumba ukiashiria kuanza kwa msimu mpya wa ligi.

Mbali na mechi hiyo, Mtibwa pia ina kibarua cha kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu ujao endapo itatimiza masharti yaliyowekwa na Shirikisho la Soka Afrika, (CAF).