Waamuzi wa kike kuchezesha AFCON-U17 kwa mara ya kwanza

|
Waamuzi wa kike walioteuliwa kuchezesha AFCON-U17 itakayofanyika nchini Tanzania mwezi Aprili mwaka huu.

Kwa mara ya kwanza, waamuzi wa kike watachezesha fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Afcon-U17) baada ya Kamati ya waamuzi ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kutaja majina ya waamuzi 29 wakiwemo watatu wa kike watakaochezesha fainali za mwaka huu zitakazofanyika nchini Tanzania mwezi Aprili.

Waamuzi waliopata bahati hiyo ni Jonesia Rukyaa kutoka Tanzania ambaye ni mwamuzi pekee wa kike katika orodha ya waamuzi 15 wa katikati walitangazwa leo.

Wengine ni waamuzi wasaidizi Mary Njoroge kutoka Kenya na Lidwine Rakotozafinoro kutoka Madagascar ambao ni waamuzi pekee wa kike kwenye orodha ya waamuzi wasaidizi 14 waliotangazwa leo.

Waamuzi hao watahudhuria mafunzo maalum yatakayoanza Machi 31 hadi Aprili 4, 2019 nchini Morocco.

Mataifa yatakayoshiriki fainali hizo ni Tanzania, Nigeria, Angola na Uganda yaliyopangwa Kundi A, wakati Guinea, Morocco, Senegal na Cameroon, zikiwa kundi B.

CAF
Maoni