Wagosi wa Kaya waibana Yanga Mkwakwani

|
Kadi nyekundu ikielekezwa kwa Issa Abushehe wa Coastal Union.

Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga SC ya Dar es Salaam, leo wameambulia pointi moja wakilazimisha sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

Wenyeji Coastal Union ndiyo waliotangulia kupata bao dakika ya 30 kupitia kwa Haji Ugando aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Ayoub Lyanga, huku Yanga wakisawazisha dakika ya 76 kupitia kwa Deus Kaseke akimalizia pasi ya Matheo Anthony.

Katika mchezo huo Coastal Union walikumbana na pigo kwa mshambuliaji wake Issa Abushehe kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga teke kwa makusudi mchezaji wa Yanga na dakika moja baadaye Yanga wakasawazisha.

Dakika ya 81, mshambuliaji wa Coastal Union Andrew Simchimba alianguka ndani ya eneo la hatari la Yanga na kudai penati lakini mwamuzi hakutoa penati na alimuonesha kadi ya njano akimaanisha kuwa Simchimba alijiangusha. 

Dakika ya 40 ya mchezo, beki wa Yanga Abdallah Haji Shaibu ‘Ninja’ alionekana kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union lakini mwamuzi hakuliona tukio hilo, na dakika ya 7 Yanga walitikisa nyavu za Coastal lakini mwamuzi aliamua kuwa ilikuwa ni off side.

Kwa matokeo hayo Yanga inaendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi 54, huku Coastal Union wakipanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya 8.

TPL
Maoni