Yanga vitani leo kuivaa Rayon Sports

|
Yanga SC vs Rayon Sports itakuwa LIVE ZBC 2 kuanzia saa 1:00 usiku.

Yanga Sc inateremka Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Saa 1:00 usiku wa leo kumenyana na Rayon Sport ya Rwanda katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mchezo huo, Yanga SC watamkosa kiungo wao, Said Juma ‘Makapu’ ambaye atakuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano na Papy Tshishimbi ambaye bado hajawa fiti kwa mchezo.

Mechi hiyo inachezeshwa na waamuzi kutoka Angola, Helder Martins De Carvalho atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Ivanildo Meirelles De O Sanche Lopes na Wilson Valdmiro Ntyamba.

Yanga itaingia kwenye mechi hiyo ikitoka kucheza mechi saba bila ya ushindi, tangu waliposhinda Aprili 7, mwaka huu walipoichapa 2-0 Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi chini ya aliyekuwa kocha wao, Mzambia George Lwandamina.

Yanga ilianza vibaya mechi za makundi Kombe la Shirikisho Mei 6 kwa kufungwa mabao 4-0 na wenyeji, U.S.M. Alger Uwanja wa Julai 5, 1962 nchini Algeria wakati Rayon ililazimishwa sare ya 1-1 na Gor Mahia siku hiyo mjini Kigali.

CAF
Maoni